Yaliyomo
- Fasili ya fasihi
- fasili ya uhakiki
- Vipengele vya uhakiki wa kazi za fasihi
- Fani
- Maudhui
Fasihi ni sanaa inayo tumia lugha katika
kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyo kusudiwa (Taasisi ya Elimu Tanzania, 1996). Haji (1983:30) fasihi ni sanaa itumiayo maneno
ili kutoa picha halisi ya mwanadamu akiwa maishani mwake; mahusiano yake na
viumbe wengine, migogoro yake na
mazingira, shida zake, raha zake, matumaini yake na jinsi anavyopiga hatua katika maendeleo yake. Fasihi ni kazi ya sanaa itoayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya kutamka au kuandika ili kufikisha ujumbe kwa jamii. Fasihi ni sanaa inayotumia lugha ili kufikisha ujumbe kwa jamii fulani (tunuzakiswahili.blogspot.com). Fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia maneno katika kufikisha ujumbe kwa jamii, kuburudisha, kuonya, kukejeri, na hata kukashifu (www.shuledirect.com). Fasihi ni sanaa inayotumia ishara (maneno au matendo) kutoka picha halisi ya maisha kwa njia bunifu na inayofuata mpangilio maalumu na lugha ya kifasaha ili kuiathiri hadhira husika (Ntarangwi, 2004). Hivyo basi fasihi ni kazi ya sanaa itoayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya kutamka au kuandika ili kufikisha ujumbe kwa jamii.
mazingira, shida zake, raha zake, matumaini yake na jinsi anavyopiga hatua katika maendeleo yake. Fasihi ni kazi ya sanaa itoayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya kutamka au kuandika ili kufikisha ujumbe kwa jamii. Fasihi ni sanaa inayotumia lugha ili kufikisha ujumbe kwa jamii fulani (tunuzakiswahili.blogspot.com). Fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia maneno katika kufikisha ujumbe kwa jamii, kuburudisha, kuonya, kukejeri, na hata kukashifu (www.shuledirect.com). Fasihi ni sanaa inayotumia ishara (maneno au matendo) kutoka picha halisi ya maisha kwa njia bunifu na inayofuata mpangilio maalumu na lugha ya kifasaha ili kuiathiri hadhira husika (Ntarangwi, 2004). Hivyo basi fasihi ni kazi ya sanaa itoayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya kutamka au kuandika ili kufikisha ujumbe kwa jamii.
Uhakiki ni kitendo cha kutathimini, kueleza,
kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida
maalumu (Ntarangwi, 2004). Uhakiki ni uchunguzi wa kazi ya kifasihi kwa
makini na kwa utaalamu. Uchunguzi wa aina hii huchunguza uchanganuzi, fasiri,
uelezaji, ufafanuzi, tathimini na utoaji wa kauli ya kijumla (Wamitila, 2002). Uhakiki ni utathmini, ufasili na uainishi wa kazi za fasihi, haumaanishi kutafuta makosa ya kazi hiyo(Peck & Coyle). Kwa hiyo, Uhakiki ni kitendo cha kuchambua, kutathmini na kuainisha kazi ya fasihi ili kuona ubora na udhaifu wa kazi hiyo kwa kutumia kaida au vigezo husika vya fani na maudhui.
Katika uchambuzi na uhakiki wa kazi za fasihi
kuna vipengele vikuu viwili ambavyo ni;
MAUDHUI
Maudhui ni kile kinachosemwa katika kazi ya fasihi (Ntarangwi, 2004). Maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusainii kazi fulani ya kifasihi (www.shuledirect.com). Maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa katika kazi ya fasihi. Hivyo tutaanza kwa kuchambua vipengele vya maudhui ambavyo hujumuisha dhamira, ujumbe, migogoro, mtazamo, na falsafa.
Dhamira ni ile jumla ya maana anayoivumbua mwandishi
aandikapo, na jumla ya maana anayoitambua msomaji katika usomaji wake
(Wamitila, 2002). Dhamira
hutumiwa kurejelea mada ya kazi fulani au ujumbe au lengo la kazi hiyo.
Kifasihi kuna aina mbili za dhamira yaani dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
- Dhamira kuu ni kiini cha kazi ya fasihi, ni wazo kuu, ni jambo linalomsukuma msanii kuandika kazi yake ili aweze kuufikisha ujumbe wake kwa hadhira.
- Dhamira ndogondogo, ni mawazo madogomadogo ambayo hujenga dhamira kuu.
Mifano
ya dhamira ni kama zifuatazo kutoka katika kazi mbalimbali za kifasihi ambazo
ni;- Kutoka katika Tamthiriya ya Amezidi
kilicho andikwa na Said Mohamed
dhamira zilizomo ni kama vile Ulevi, mwandishi ameizungumzia katika uk 50
anasema “wanakunywa wisky…” . Na
dhamira nyingine ni kama vile Umasikini na Matabaka uk 60. Tamthiriya ya Nguzo Mama iliyoandikwa na Penina Mhando ameelezea dhamira
mbalimbali kama vile dhamira ya Ukombozi wa mwanamke, kama ilivyoelezwa na
mwandishi kwa kumtumia “Bi Nane; Basi
tusikilizane. Mnajua Nguzo Mama haiwezi kusimama mpaka tuivute kwa kamba”. Pia katika riwaya ya Kufirika mwandishi Shaban Robert ameonesha dhamira kuu ni Ukombozi wa kiutamaduni.
Kiujumla riwaya ya kufikirika
inajadili harakati zinazofanywa na Utu Busara za kupambana na tamaduni
zilizopitwa na wakati. Pia mwandishi amejadili dhamira ndogondogo kupitia
wahusika lukuki ambao amewatumia katika riwaya hii, Dhamira hizo ni kama
zifuatazo: Suala la uongozi, Suala la ugumba na
utasa,
Mgogoro ni hali ya kutokuelewana baina ya pande mbili yaani
mtu na mtu, mtu na kikundi au mtu mwenyewe na nafsi yake. Migogoro ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi
za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao au matabaka yao.
Migogoro hii inaweza
kugawanywa katika vipengele vifuatavyo;
- mgogoro wa nafsi,
- mgogoro wa kijamii,
- mgogoro wa kiuchumi
- mgogoro wa kisiasa.
Ujumbe ni funzo na
maadili yaliyokusudiwa na mtunzi yaifikie jamii aliyoilenga kufikisha kazi yake
ya fasihi. Katika riwaya ya Kufikirika
iliyoandikwa na Shaaban Robert kupitia dhamira mbalimbali zimeweza kutuibulia
ujumbe ufuatao; Umoja ni nguvu na
utengano ni udhaifu. Mfano wananchi wa kufikirika walikuwa na umoja katika
kufanikisha ustawi wa nchi yao hali kadhalika watu wa kufikirika walikuwa na
umoja na ushirikiano katika kufanikisha mfalme wao anapata mtoto. Kwenye upendo, umoja na ushirikiano hakuna
vurugu na matatizo mbalimbali.
Ustawi wa nchi ya Kufikirika umetokana na umoja na ushirikiano waliokuwa nao,
na Jamii isijiegemeze katika imani za
kimila na kitamaduni tu bali iangalie upande mwingine. Hii inatokana na
ukweli kwamba wanakufikirika walikuwa hawaamini masuala ya hospitali badala
yake walikuwa wanaamini mambo ya kimila na kitamaduni. Pia katika Riwaya ya Kusadikika iliyoandikwa na Shaaban Robert ameonesha ujumbe kama, Uongozi
mbaya unachangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maendeleo ya
wananchi, kuwa na tamaa na viongozi
kujali maslahi binafsi kunapelekea hali
duni ya wananchi walio wengi na
Viongozi wanapaswa kuthamini haki za wananchi wanaowatumikia. Pia kutoka
katika Tamthiriya ya Nguzo Mama
iliyoandikwa na Penina Mhando
ameonesha ujumbe mbalimbali kama vile, Umoja
ni nguvu, Umuhimu wa ukombozi wa mwanamke, na Uongozi bora ni chachu ya maendeleo.
Falsafa, kiujumla falsafa ni mchujo wa welekeo wa
mawazo muhimu yajitokezayo kila mara katika kazi mbalimbali za msanii ( Senkoro,
2011). Falsafa ni imani na mwelekeo wa
mwandishi kuhusu maisha. Kutoka
Riwaya ya Kusadikika iliyoandikwa na Shaaban Robert falsafa ya mwandishi ni ya “wema hushinda ubaya”, amedhihirisha
hili kupitia mhusika Karama aliyechorwa kama mtu mwema dhidi ya Majivuno
aliyechorwa kama mtu mbaya. Kwa taswira hii Karama amewakilisha wema wote
katika jamii ya wasadikika na Majivuno anawakilisha wabaya wote katika jamii
hiyohiyo. Pia katika kitabu cha
Riwaya za Rosa Mistika, Mzingile na
Nagona ziliyoandikwa na Kezilahabi falsafa yake ni “Maisha hayana maana”. Pia kutoka katika Tamthiriya iliyoandikwa na
Penina Mhando ya Nguzo Mama mwandishi anaamini kwamba “Mwanamke ukimwezesha anaweza”.
Msimamo wa mwandishi, msimamo ndio
uwezo wa kuwatofautisha wasanii wawili wanaotunga kazi za fasihi zilizo na
kiini na chimbuko moja ( senkoro, 2011). Katika riwaya ya Kufikirika mwandishi Shaaban
Robert anaonekana kuwa na msimamo wa kiyakinifu. Kwa mujibu wa mwandishi
anaona katika kipindi cha sayansi na teknolojia mila na tamaduni za zamani
zisipewe nafasi. Kutoka katika riwaya ya Kusadikika msimamo wa mwandishi Shaaban Robert ni wa kimapinduzi, kwani
anaonesha jinsi jamii ilivyopaswa kujituma tena kwa ujasiri, kupigania haki na
mabadiliko ya wananchi wote. Katika
tamthiriya ya Nguzo Mama msimamo wa mwandishi, Penina Mhando ni wa kimapinduzi, kwani anajaribu kuiaminisha jamii
na kuibadirisha kifikra kutoka kutomwamini na kutomthamini mwanamke na kuanza
kujenga imani juu yao. Mfano amemchora mhusika Bi- Nane kama mtu mwenye msimamo na mpenda maendeleo.
FANI
Fani katika fasihi ni ule ufundi wa kisanaa
anaotumia msanii katika kazi yake (Senkoro 2011). Fani
ni ufundi wa msanii katika kuumba umbo la kazi ya fasihi kutokana na ubunifu
wake. Fani ni ufundi ambao msanii anautumia katika kufikisha ujumbe kwa jamii. Katika fani msomaji anatakiwa kuzingatia;
- Muundo au mtiririko(ploti) wa kazi
- Mtindo alioutumia mwandishi katika kazi yake
- Lugha - mwandishi ametumia lugha namna gani
- Madhari
- Wahusika - jinsi mwandishi alivyo wasawili wahusika wake
- Usimulizi wa kazi za fasihi
Wahusika ni binadamu wanaopatikana katika kazi
ya kifasihi na ambao wanasifa za kimaadili, kitabia, kiitikadi na kifalsafa
ambazo hutambulishwa na wanayoyasema (mazungumzo) na wanayoyatenda (matendo)
(Wamitila, 2002). Mhusika katika fasihi ni kiumbe cha hadithini
kilichobuniwa na msanii ili kuendeleza hoja na maudhui yake katika kazi yake
(Ntarangwi, 2004). Wahusika ni viumbe hai au visivyo hai ambavyo
vinawakilisha watendaji halisi katika maisha ya kila siku ya jamii husika
katika kuonyesha wasifu wa ndani na nje kama vile hali ya kusononeka mhusika,
furaha au tabia fulani katika jamii inayotuzunguka. Hivyo wahusika huelezea
hali halisi ya maisha ya jamii. Iwe mitaani, iwe sehemu za kazi, iwe shuleni na
kwingineko ambako kunahusisha mikusanyiko ya watu wa tabia tofauti tofauti. Mhusika husaidia katika kuendeleza mada nzima
anayoizingatia msanii hususa kwa kufululiza vitushi na visa mbali mbali katika
kazi ya msanii ili kuwafikia wasomaji au wasikilizaji wake. Mhusika hupewa maneno,
dhana, na hulka ambazo ni muhimu katika kujenga hadithi, dhamira, na maudhui ya
kazi ile. Wahusika wanakusudiwa kutenda matendo, tabia au matukio halisi katika mazingira halisi. Wahusika wamegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni wahusika wakuu na wahusika wasaidizi.
- Wahusika wakuu ni wale wanaobeba dhamira kuu katika kazi ya fasihi. Hawa ndiyo vipaza sauti vya mwandishi. Wahusika hawa huonekana kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho wake.
- Wahusika wadogo au wasaidizi ni wale ambao wanajitokeza hapa na pale katika kazi ya fasihi ili kukamilisha ulimwengu wa kazi hiyo. Wahusika hawa hutumiwa na mwandishi katika kukuza dhamira. Wahusika wadogo wamegawanyika katika aina mbalimbali. Wako wahusika bapa, Mviringo,Kinyago, Jumui, Batili, Foili na wahusika Kikalagosi.
Mfano
katika Riwaya ya Kufikirika mwandishi
Shaaban Robert amewatumia wahusika
mbalimbali katika kuibua au kuunda
dhamira zake. Baadhi ya wahusika aliowatumia ni kama Mfalme, huyu alikuwa
ndiye kiongozi au mfalme wa nchi ya Kufikirika ambaye aliongoza vema na alikuwa
mtu mwenye huruma na upendo na watu wake. Hali kadhalika mfalme alikuwa ni
jasiri na mzalendo aliyepigania haki. Malkia,
huyu alikuwa ni mke wa mfalme ambaye pia alikuwa anasumbuliwa na tatizo la
utasa, ni mwanamke mvumilivu na mwenye subira, hivyo mwandishi kwa kumtumia
mhusika Malkia ameibua dhana ya utasa na uvumilivu. Utu busara ujinga hasara, ni mhusika aliyeibua dhamira nyingi
katika riwaya hii ya kufikirika, alikuwa ni mtu makini na mwenye upeo mkubwa
katika kufikiria mambo. Huyu ndiye aliyetabiri kuzaliwa kwa mtoto wa mfalme,
baadaye akawa mwalimu wa mtoto wa mfalme na baadaye akajiingiza katika ukulima (uk 49). Pia katika Tamthiliya ya Nguzo Mama mwandishi Penina Mhando amewachora wahusika
mbalimbali ili kufikisha ujumbe aliokusudia kwa msomaji. Wahusika hao ni kama
vile, Bi-Pili ambaye alikuwa ni
mpishi wa pombe, ni mpenda maendeleo na pia ni mke wa Sudi na mlezi wa familia. Bi-Nne huyu ni mhusika mkuu, ni mwenye wivu
asiyependa maendeleo ya wenziwe, na ni mwenyekiti wa kamati ya mashauri. Bi-
Nane ni msomi, ni mpenda
maendeleo, na ni mvumilivu. Kitabu kingine ni Riwaya ya Amezidi mwandishi Shaaban
Robert amewatumia wahusika kama, Ame
na Zidi hawa ni wahusika wakuu katika
kazi hii. Wahusika wengine wadogowadogo ni Mari,
Joice, na Jane. Kutoka katika
tamthiliya ya Kwenye Ukingo Wa Thim kilicho andikwa na Ibrahim Hussein yeye amewatumia wahusika wafuatao ili kufikisha
ujumbe kwa wasomaji wake, Abert na Marther ambao ni wahusika wakuu katika
tamthiliya hii na wengine wadogowadogo ni kama vile;- Kriss, George, Ridia, Jine, na Stella.
Muundo hutokana na umbo na mpango wa kazi ya
fasihi; kwa hiyo hapa ndipo tutapata katika ushairi wa Kiswahili, mashairi
yenye miundo mbalimbali iainishwayo na idadi ya mistari (vipande/mishororo)
katika kila ubeti, mathalani mashairi ya uwili, utatu, unne (Senkoro, 2011) Muundo katika kazi ya fasihi muundo ni mpango na mtiririko
wa kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio (Senkoro 2011). Muundo ni namna matukio katika kazi ya fasihi yalivyopangwa na kuleta
mtiririko wa kazi husika ya fasihi. Muundo ni mtiririko wa kazi ya fasihi kwa upande wa visa na matukio. Kinachozingatiwa hapa ni jinsi mwandishi alivyopanga kazi yake mfano sura na sura, kisa na kisa au tukio na tukio. Muundo unaweza ukawa wa aina zifuatazo.
- Muudo sahili.- Muundo wa moja kwa moja
- Muundo wa urejeshi-Muundo wa kuanzia mwisho-kati-mwanzo au kinyume chake.
- Muundo wa duara
- Muundo changamani- huwa na matukio/hadithi tofauti tofauti ndani ya hadithi au kisa kimoja.
- Muundo mpalaganyiko.
Hivyo
katika riwaya ya Nagona mwandishi E. Kazilahabi ametumia muundo wa “Rejea”
ambapo mwandishi ameanza na kisa cha mbele katika kazi yake. Kutoka katika
Tamthiliya ya Nguzo Mama mwandishi
ametumia muundo wa “moja kwa moja” (sago) ambapo amepanga matukio au visa vyake
kwa mtiririko kutoka onesho la kwnza hadi la nne. Kitabu kingine ni kile cha Kufikirika mwandishi Shaaba Robert ametumia muundo wa “moja kwa moja” ambapo amesimulia kitabu
mwanzo hadi mwisho. Kwa kuigawa kazi yake katika sehemu ndogondogo, kwakuzipa
vichwa vya habari kama vile Mfalme,
Waganga, Matokeo ya utabiri, Mtoto wa mfalme na Kafara. Pia sura ya
tano ameigawa katika sehemu kuu mbili na kuipa jina la Baraza na Gereza.
Mtindo, katika kazi ya fasihi ni ile nama
mbayo msanii hutunga kazi hiyo na huipa sura ambayo kifani na kimaudhui
huainisha kanuni au kawaida zilizofuatwa kama ni zilizopo (za kimapokeo) au ni
za kipekee (senkoro 2011). Mtindo ni upekee wa uundaji wa kazi ya fasihi na hutofautiana baina ya
msanii mmoja na mwingine kulingana na hisia za msanii huyo. Utofauti huo
unaweza kujitokeza kwenye matumizi ya nafsi, uteuzi wa msamiati, mwanzo na
mwendelezo wa kazi yake, usimulizi wa mwandishi, uchanganyaji wa tanzu
mbalimbali za fasihi, kama vile kuingiza kipengele cha wimbo katika kazi ya
fasihi andishi.
Katika Tamthiliya ya Nguzo Mama
mwandishi Penina Mhando ametumia
mtindo wa “majibizano (dialojia) (uk 36-
37), mtindo wa “monolojia” (uk 13 na35),
mtindo wa nafsi zote tatu mfano; Nikianza
kuyasimulia nafsi ya kwanza, Nawewe
wajua kupika nafsi ya pili, na ile ya tatu ambayo ni Wakaanza kuinua. Katika Riwaya ya Kufikirika Mwandishi Shaaban
Robert katika kazi yake hii ametumia
mtindo wa “masimulizi” yaani amesimulia matukio yote katika mtiririko unaofaa,
pia “nafsi zote tatu zimetumika”, hali kadhalika mwandishi ametumia “ushairi” (uk 18-19). Pia ametumia mtindo wa kutoa
maana ya meneno magumu mwishoni. Pia katika Riwaya ya Kusadikika Mwandishi Shaaban
Robert ametumia mitindo mbalimbali katika kazi hii kama vile, ametumia
“maswali” hasa katika sehemu ya mwisho ya kitabu, ametumia “diolojia” kati ya
Sapa na Salihi (uk. 29), ametumia
“masimulizi” kwa kiasi kikubwa, na matumizi ya “nafsi ya pili na tatu umoja na
nafsi ya tatu wingi” sehemu kubwa ya kazi yake.
Mandhari huwa ni sura ya mahali hususa jinsi
panavyoonekana katika hali halisi ya maisha. Mtunzi anaweza kutumia mandhari
kueleza mazingara halisi ya kisa anachosimulia katika kazi yake. Mathalani,
mtunzi anaweza kutuchorea mandhari ya pwani kwa kushughulikia vitu kama vile
upwa na ziwa, minazi, nyumba za makuti n.k. Jambo hili huleta hali ya ufasaha
katika utunzi (Ntarangwi, 2004). Mandhari ni ile arki au elementi ambayo hutufichulia
wapi na lini ambapo matukio fulani yalifanyika (Wamitila, 2002). Mandhari ni mahali ama
wakati tukio la kifasihi lilivyobuniwa na kutendeka na msanii na hivyo
hufanikiwa kujenga hisia ya msomaji au msikilizaji ama mtazamani kulingana na
kazi yake ya fasihi aliyoiandaa. Mandhari ni sehemu ambayo kazi ya fasihi ilitendeka, inatendeka au itatendeka. Kazi ya fasihi iwayo yote ile lazima iendane na mandhari husika. Aidha mada au jambo linalozungumzwa sharti iendane na sehemu au mahali ambapo tukio hutokea. Madhari hutumika kulejelea wakati na sehemu matukio ya msuko hutokea.
Kwa mfano katika riwaya ya kufikirika mwandishi Shabani
Robert ametumia mandhari ya kufikirika, kwani hata nchi inayozungumziwa ni
ya Kufikirika, pia nchi zilizopakana na nchi ya Kufikirika nazo ni za
kufikirika. Pia mwandishi ametumia muktadha halisi kama vile Gerezani, Nyumbani
kwa Mfalme, Bustanini (uk 1) na
Shambani. Kupitia mandhari hizi mwandishi, Shabani
Robert ameibua dhamira mbalimbali. Katika kitabu cha Kusadikika
mwandishi ametumia mandhari ya Kufikirika
ambayo haiwezi kuonekana kwa macho ya kawaida kwani ni nchi inayoelea angani.
Pia ametumia mji wa Sadiki na mipaka au pande sita zinazopakana na nchi hii za
Kaskazini, Mashariki, Kusini, Magharibi, Ardhini na Mbinguni. Pia kitabu cha tamthiliya ya Nguzo Mama mwandishi ametumia mazingira
halisi kwani ni ya kijijini.
Matumizi ya lugha ni namna ambavyo
msanii ameteua na kupangilia tamathali za semi kama sitiari, tashbiha, takriri,
tashihisi na tafsida, methali, misemo,
taswira,nahau, lugha za kigeni na kadhalika.
Matumizi ya lugha, hujumuisha jinsi mtunzi alivyotumia lugha katika
kuwasilisha kazi yake. Matumizi ya lugha hujumuisha misemo, nahau, methali na
tamathali za semi. Mifano ya matumizi ya lugha kutoka kazi mbalimbali za
kifasihi ni kama ifuatayo;- Katika kitabu cha riwaya cha Kufikirika mwandishi ametumia lugha ya, Methali,
methali zilizotumika katika riwaya hii ni kama vile, nyumba ya mgumba haina matanga
(uk 5), mwenye haya hazai (uk 6), asiye kubari kushindwa si mshindani” (uk 27).
Kutoka katika kitabu cha Kusadikika
mwandishi Shaaban Robert ametumia methari kama, Kitanda usichokilalia hujui Kunguni wake, Msiba wa kujitakia
hauna kilio, Lila na fila hawatangamani. Pia katika tamthiliya ya Nguzo Mama mwandishi ametumia methari
zifuatazo katika kazi yake, Umoja ni
nguvu utengano ni udhaifu (uk 30), Lamgambo likilia lina jambo (uk 4), Aso
mwana aeleke jiwe (uk 4). Misemo, Katika riwaya ya Kufikirika misemo iliyotumika ni kama
ifuatayo;- Dunia haifichi siri (uk 23), maisha ni kama kuwa katika bahari (
uk 24). Kitabu cha Nagona mwandishi
ametumia misemo kama Fikra hufumba mboni
za urazini (uk 14) Pia kutoka katika tamthiliya ya Nguzo Mama mwandishi ametumia misemo kama, Ukilikoroga pumba nakula utalila (uk 26), Utakufa kibudu (uk 23),
Akachanganya ulimi (uk 57). Katika kitabu cha Kusadikika mwandishi
ametumia misemo mbalimbali kama vile, kumtosa
mshitakiwa katika bahari ya maangamizi. Tamathali za semi, haya ni maneno ambayo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili
kutia nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi au kusema. Pia
tamathali za semi hutumika ili kupamba lugha au mazungumzo. Mfano katika riwaya
ya Kusadikika mwandishi Shaaban
Robert ametumia tamathali mbalimbali kama zifuatavyo:- Tashibiha, katika riwaya hii tashibiha zilizojitokeza ni kama vile kichwa chake kilishindiliwa kama gunia (uk
29), Sauti ya waafrika ni kali kama
ile ya radi (uk 6), Waliweza kunusa kama mbwa mwitu (uk 8), Akili yake kali
kama wembe (uk 38), Maswali aliyamimina kama maji (uk 29). Kutoka katika
kitabu cha Amezidi mwandishi ametumia tashibiha kama vile; Mkono wangu mrefu kama ule wa Shetani (uk 8). Kitabu cha Mzingile kuna tashibiha kama Uogaji wangu haukuwa kama wa ndege (uk 7). Kitabu
cha Nguzo Mama mwandishi ametumia
tashibiha kama Amevaa kama mkulima wa
bara (uk 24), Wanasagwa kama mbuzi (uk 32), Anatembea kama amepigwa na bumbuazi
(uk 8). Sitiari ni tamathali ya semi ambayo
hulinganisha vitu viwili au zaidi bila kutumia maneno kama, au mithili ya.
Katika tamthiliya ya Amezidi
mwandishi Said Mohamed ametumia sitiari kama vile; Tuwe simba basi (uk 72). Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo, mwandishi Kezilahabi ametumia sitiari kama vile “Huyu ni baba yako.” (uk.12) pia “Ujamaa ni mzuri.’ (uk.112) Takriri ni tamathali ya semi ambayo neon
hujirudiarudia kwa lengo la kusisitiza jambo fulani. Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo mwandishi Kezilahabi ametumia sitiari katika
sehemu mbalimbali mfano “Haa! Haa!
Haa!”(uk.12), “Mauti mauti” (uk.17). Pia katika tamthiliya ya Amezidi mwandishi Said Mohamed ametumia takriri mfano “mumu mumu” (uk.75), “Joto…joto...ndani
joto na nje joto” (uk.36).
Tashihisi, hapa vitu visivyo na sifa walizonazo watu hupewa sifa hizo.
Katika kitabu cha Nagona mwandishi
amezionesha kama ifuatavyo; Bonde la
hisia (uk 16), bonde la mvi (uk 18). Kitabu cha Vuta N`Kuvute mwandishi ametumia tashihisi zifuatzo; Nuru ya jua iliingia kwa hamaki chumbani mle
na ilikashifu uchafu wote wa chumba kile (uk 49). Kitabu cha Kufikirika mwandishi Shaaban Robert ametumia tashihisi
zifuatazo, Sauti ya ndege waliokuwa
wakiimba matawini kwa kuagana na mchana ilikuwa na simanzi masikioni (uk 1). Katika
kitabu cha Kusadikika tashibiha
zilizotumika ni kama vile; Giza limezalo
nuru na ufupisho uoni wa macho, Wakati
una mabawa kama ndege (uk. 11). Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo, Kezilahabi
pia ametumia tashihisi mfano “kila
jiwe walilokalia liliwaambia samahani umekalia bega langu.”(uk.32)
Mubalagha, ni tamathali ya semi ambayo hutia chumvi au hukuza jambo.
Katika riwaya ya Kufikirika mwandishi
ametumia mbinu hii katika (uk
11) siku hiyo kuni, mkaa, na mafuta yote yalikwisha kwa kuchoma hirizi
hizo, moshi mwingi uliruka juu ukatanda katika hewa kama wingu kubwa la mvua.
Matumizi ya lugha za kigeni, hizi ni lugha azitumiazo mwandishi
katika kazi yake ya kifasihi ili kufikisha ujumbe na kumburudisha msomaji wa
kazi yake. Mfano wa lugha hizo zilivyo tumika katika kazi za kifasihi ni kutoka
kitabu cha Amezidi mwandishi ametumia
maneno ya lugha ya kiingereza kama “How
do you do? All right! (uk 60)”, Cheers! (uk 58), Entertainment (uk 49). Pia
katika kitabu cha Mzingile mwandishi
ametumia maneno ya lugha ya kiingereza kama well
done! (uk 40). Kitabu cha Nguzo Mama
mwandishi ametumia maneno ya lugha ya kiingereza kama vile, My God, Degree. Aidha katika riwaya ya
Dunia Uwanja wa Fujo mwandishi Kezilahabi ametumia lugha ya Kiingereza, mfano “Welcome
back” (uk.88). “Security (uk.89 - 90).” Snow cap” (uk.62)
Pia lugha ya picha, waandishi wengi wa kazi za kifasihi hutumia lugha za picha
ili kupunguza au kuficha baadhi ya mambo yasionekane dhahiri kwa mlengwa
mwenyewe, au kuwakilisha tabia za watu katika jamii. Mfano kutoka katika kazi
za kifasihi ni kama vile;- Katika kitabu cha Nagona mwandishi ametumia lugha ya picha kama Kamasi, na funza (uk 16), vinyesi (uk 19), nyuki (uk 56). Kitabu
cha Mzingile mwandishi ametumia lugha
ya picha kama Mjusi (uk 46). Kutoka
kitabu cha Nguzo Mama mwandishi
ametumia kamba, nguzo mama.
Kwa
ujumla uchambuzi na uhakiki wa kazi mbalimbali za kifasihi humsaidia msomaji wa
kazi husika ya kifasihi kuielewa au kupata mwanga fulani juu ya kazi husika
aisomayo. Aidha kazi ya uhakiki hufanywa na mhakiki wa kazi ya fasihi ambaye
ndiye hufanya kazi kubwa ya kuchanganua kazi mbalimbali za kifasihi ili ziweze
kumrahisishia msomaji kuzielewa kwa ufasaha kazi husika.
MAREJEO
Ameir, I.H
(1983) Misingi ya Nadharia ya Uhakiki. Dar es Salaam: Tuki
Hussein, E.(1988). Kwenye Ukingo wa Thim, Nairobi,Oxford
University Press East Africa Ltd.
Kezilahabi,
E. (1990) Nagona, Dar es Salaam, Dar
es Salaam University Press.
Kezilahabi,
E. (1991) Mzingile, Dar es Salaam,Dar
es Salaam University Press.
Kezilahabi,
E. (2007) Dunia Uwanja wa Fujo, Nairobi,
Vide Muwa Publishers
Mhando
P. (1982) Nguzo Mama, Dar es Salaam,
Dar es Salaam University Press.
Mohamed
S.A (1995) Amezidi, Dar es Salaam,
East African Educational Publishers.
na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili
(TUKI).
Ntarangwi, M. ( 2004). Uhakiki Wa Kazi Za Fasihi. Augustana College, Rock Island, IL612
Publishers Ltd.
Robert, S (1991) Kufikirika, Dar es salaam, Mkuki na
Nyota Publishers.
Robert, S. (1991) Kusadikika, Dar es Salaam, Mkuki na Nyota Publishers.
Senkoro, F.E.M.K (2011) Fasihi, Dar es salaam, KAUTTU.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la Pili). East Africa: Oxford
University Press
Wamitila K. W, (2002), Uhakiki Wa Fasihi Misingi Na Vipengele Vyake, Nairobi, Phoenix
Kazi nzuri
ReplyDeleteKazi Bora. Heko!
ReplyDeleteKazi nzuri... Kongole kwako mwandishi....!!!
ReplyDeleteKazi nzuri sanah
ReplyDeleteKazi ya kuvutia sana ...heko kwako
ReplyDeletekazi nzuri hii..
ReplyDeleteKazi safii na marejeleo bombaa
ReplyDeleteKazi safi na marejeleo bomba
ReplyDeleteNashukuru kwa kazi kuntu kama hii. Imenisaidia katika ufunzaji
ReplyDeleteThanks na vigezo zake
ReplyDeleteKazi safi🙏
ReplyDeleteUmuhimu wa migogoro?
ReplyDelete🤝👏👏👏
ReplyDeleteKongole sana kwa kazi nzuri
ReplyDelete